24 Machi 2020 - 06:52
Angela Merkel ajiweka karantini baada ya kugusana na daktari aliyekuwa na Corona

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amechukua uamuzi wa kujiweka karantini baada ya kufahamika kwamba, daktari aliyemtibu ameambukizwa virusi vya Corona, huku maambukizo ya virusi hivyo yakienea kwa kasi barani Ulaya.

(ABNA24.com) Duru za karibu na Kansela huyo wa Ujerumani zinasema kuwa, baada ya vipimo kuonyesha kuwa, dakrati aliyemtibu ameathirika na virusi vya Corona, Bi Angela Merkel amejiweka karantini nyumbani kwake mpaka majibu ya vipimo vyake yatakapohamika.

Taarifa zinakuja siku moja tu baada ya serikali ya nchi hiyo kupiga marufuku mikusanyiko, huku hoteli zikiruhusiwa kufanya kazi kwa sharti la kutoa chakula cha kubeba na kwenda kula nyumbani.

Karibu watu 25,000 wameambukizwa virusi vya Corona nchini Ujerumani huku vifo vya watu 94 vikiwa vimesharipotiwa.

Nchini Italia hali ni mbaya zaidi ambapo hadi sasa karibu watu 60,000 wameshaambukizwa virusi vya Corona 5,476 wamefariki dunia, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa na rekodi kubwa zaidi ya vifo vya Corona.

Aidha nchini Uhispania maambukizo ya virusi vya Corona yanaenea kwa kasi ambapo hadi sasa watu takribani 29,000 wameambukizwa na 1,772 wamefariki dunia.

Aidha ripoti kutoka nchini Ufaransa zinasema kuwa, watu karibu 17,000 wameambukizwa virusi vya Corona nchini humo huku 674 wakiaga dunia.

Marekani nako hali inazidi kuwa mbaya ambapo watu wasiopungua 35,000 wameambuukizwa virusi vya Corona na karibu 500 wamefariki dunia.

Nchini Uingereza pia walioambukizwa virusi vya Corona wamekaribia 6,000 na hadi sasa watu 281 wamefariki dunia nchini humo kwa maradhi hayo.

.............
340